AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

IDARA ZA CHAMA CHA MAPINDUZI


x
alternative
Ndugu. Issa Haji Ussi (Gavu)
Katibu wa NEC Organizesheni

IDARA YA ORGANAIZISHENI

Idara ya Organaizesheni ni moja kati ya Idara nne za CCM. Idara hii imeanzishwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya Mwaka 1977 Toleo la 2017 Ibara ya 107 (1).

Idara hii ndiyo injini ya Uendeshaji wa Chama kwani ndio Idara inayohusika na Masuala yote ya Wanachama; kwani Chama kisicho na Wanachama ni sawa na gunia tupu ambalo haliwezi kusimama. Idara hii ndio inayoshughulika na Vikao na Maamuzi ya vikao. Kwa kuwa Chama ni muungano wa watu wenye nia na malengo yanayofanana, hivyo watu hao wanaounganishwa na Itikadi yao hufikia maamuzi ya pamoja kupitia Vikao vyao. Kwenye Chama Cha Kidemokrasia kama CCM hakuna mtu mmoja mwenye uwezo wa kufanya maamuzi ya Chama nje ya vikao. Inatosha kusema, “Hakuna Chama bila Vikao”.

Idara ya Organaizesheni ndio inayosimamia Jumuiya za Chama na Sehemu ya Wazee. CCM ilianzisha Jumuiya za CCM ili ziwe ni mkondo wa kufikisha Sera zake na Siasa ya CCM kwenye Makundi yote ya Kijamii kwa upande mmoja, na kuwa mkondo wa kuitafutia CCM Marafiki na Wanachama kutoka kwnye makundi hayo kwa upande wa pili. CCM pia inathamini sana mchango wa Wazee katika maendeleo ya Taifa letu, ndio maana ikaanzisha sehemu ya Wazee ili kuwawezesha Wazee kurithisha kwa Taifa busara, hekima na ujasiri wao ndani ya Jamii. Wahenga walisema, “Isiyo kongwe, haivushi.”

Idara ya Organaizesheni ndio inayosimamia masuala yote ya uchaguzi wa ndani ya CCM na ule wa kushika Dola. Viongozi wa Cham a cha Kijamaa huchaguliwa kwa kura za wanachama na huongoza Chama kwa ridhaa yao. Lakini pia Chama chochote cha Siasa duniani lengo lake kuu huwa ni kushinda uchaguzi ili kushika dola na kuunda Serikali. Kwa kuwa toka Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar nchi hii imekuwa chini ya Uongozi madhubuti wa CCM, ndiyo kusema Idara hii imetimiza vema majukumu yake.

Idara ya Organaizesheni ndiyo inayosimamia Katiba Muundo Kanuni, na Taratibu za Chama na Jumuiya za CCM. Hii ndiyo kusema Idara hii ndiyo inayohakikisha wakati wote kuwa Katiba ya CCM, Kanuni zote za Chama na Jumuiya zake, Muundo wa Chama na Taratibu mbalimbali zikiwemo taratibu za Sehemu ya Wazee zinakiwezesha Chama kutekeleza madhumuni ya kuundwa kwake. Idara hii ndio hufanya marekebisho ya miongozo hii kwa mujibu wa mahitaji ya Chama kwa wakati husika. Bila shaka utaona kuwa utulivu uliopo CCM ukilinganisha vyama vingine vya Siasa hapa nchini unatokana na utekelezaji mzuri wa wajibu huu.

Hii ndio sababu tukasema Idara hii ndiyo injini ya Chama. Kwani Gari lisilo na injini linawezaje kusafiri?

alternative
Ndugu. Paul C. Makonda
Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi

Idara ya Itikadi na Uenezi

  • Kushughulikia masuala ya msingi ya Itikadi na Sera za Chama Cha Mapinduzi.
  • Kueneza na kufafanua Itikadi na Sera za CCM.
  • Kupanga na kusimamia Mafunzo na Maandalizi ya Makada na Wanachama.
  • Kusimamia Vyombo vya Habari vya Chama, Mawasiliano na Uhamasishaji wa Umma kwa Jumla.
  • Kuongoza na kusimamia maandalizi ya Sera, Programu na Ilani za Uchaguzi za CCM.
  • Kusimamia Utafiti, Maktaba na Nyaraka za Chama.
alternative
Dkt. Frank George Haule Hawassi
Katibu wa NEC wa Uchumi na Fedha

Uchumi na Fedha

Idara ya Uchumi na Fedha ni miongoni mwa Idara tano za Chama cha Mapinduzi zinazoongozwa na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa ambazo zimeundwa kwa mujibu wa Ibara ya 105 ya Katiba ya CCM ya Mwaka 1977, Toleo la 2017. Idara hii inaongozwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa wa Uchumi na Fedha ambaye ni Dkt. Frank George Haule Hawassi.

Majukumu ya msingi ya Idara yameainishwa na kutajwa bayana kwenye Ibara ya 107(4) (a)-(e) ya Katiba ya CCM, kama ifuatavyo:

  1. Kufuatilia utekelezaji wa Sera za CCM za Uchumi.
  2. Kuratibu mapato ya fedha za Chama nchini kote kwa ajili ya maamuzi ya uwekezaji wa Chama.
  3. Kusimamia vitega uchumi na uwekezaji katika Chama.
  4. Kusimamia Mali za Chama nchini kote, na
  5. Kusimamia mapato na matumizi ya Chama katika ngazi zote za uongozi wa CCM.

Ili kurahisisha na kuleta ufanisi wa utendaji kazi za Chama, muundo wa Idara ya Uchumi na Fedha umegawanywa katika vitengo vitatu muhimu ambapo kila kitengo kimegawanywa pia katika sehemu (Sections) na kupangiwa majukumu mahsusi ya kila siku ya kusimamia, kufuatilia na kutekeleza. Vitengo vya Idara ni hivi vifuatavyo:

  1. Kitengo cha Fedha na Uhasibu.
  2. Kitengo cha Uchumi, Mipango na Uwekezaji.
  3. Kitengo cha Miliki.

Pamoja na majukumu ya Kiidara, Idara pia inayo majukumu mengine ya msingi ya kusimamia na kuratibu shughuli zote za Baraza la Wadhamini wa CCM kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM zikiwemo shughuli za vikao, usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa maazimio ya vikao vya Baraza la Wadhamini wa Chama Cha Mapinduzi.

Kwa kuzingatia utajiri mkubwa Chama kilionao hususan katika eneo la Rasilimali Ardhi na Rasilimali Wanachama, Idara ya Uchumi na Fedha ina wajibu wa msingi wa kuhakikisha rasilimali hizi zinatumika kikamilifu katika kukiimarisha Chama kiuchumi na kimapato hatua ambayo itakiwezesha Chama kuhudumia kwa ufanisi majukumu yake ya kisiasa na uendeshaji wa Ofisi.

alternative
Ndugu. Rabia Abdallah Hamid
KATIBU wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa

Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa

Idara ya mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ni moja kati ya Idara za CCM Makao Makuu inayoundwa na Ibara ya 107 kifungu cha 3 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la 2017.

Idara hii inafahamika zaidi kama idara inayoshughulika na kujenga uhusiano wa kimataifa, hata hivyo ukweli ni kwamba idara hii inashughulikia mambo mengi na muhimu ndani ya nchi yanayojenga taswira njema ya CCM kwa wananchi. Kwa kifupi tunasema, idara hii inajihusisha na kazi za Chama nje ya Chama ndani ya Umma.

Kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa inajukumu la msingi la kufuatilia hali ya Kisiasa Nchini. Kwa lugha nyepesi ina kazi ya kufuatia hali ya maisha ya wananchi wa Tanzania, kijamii na kiuchumi kwa ujumla.

Idara hii pia ndiyo yenye jukumu la kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM Nchini, kuona kwamba tumefanikiwa kwa kiasi gani kutekeleza Ilani yetu, ni kwa kiasi gani tumeondoa kero na changamoto zinazowakabili wananchi wetu na kukishauri Chama namna ya kukabiliana nazo. Ukiacha mbali jukumu la kufuatilia maendeleo ya Jumuiya za Kijamii nchini, na kushughulikia na kusimamia masuala ya Itifaki ndani ya Chama, Jukumu lingine kubwa na muhimu la Idara hii ni kuratibu uhusiano na ushirikiano wa CCM na Vyama vya Siasa vya Kidugu , Kirafiki na vya Kimapinduzi. Aidha, Idara ina jukumu la kufuatilia hali ya kisiasa katika nchi jirani na nchi nyinginezo duniani na kufuatilia maendeleo ya kijamii ya Kamati za Urafiki na Mshikamano kati ya Watanzania na wananchi wa nchi Rafiki.

  • Kufuatilia hali ya kisiasa nchini.
  • Kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na Sera za Kijamii za CCM.
  • Kufuatilia harakati za Vyama vya Siasa nchini.
  • Kufuatilia Maendeleo ya Jumuiya za Kijamii nchini.
  • Kuratibu uhusiano na ushirikiano wa CCM na vyama vya siasa vya kidugu, kirafiki na vya kimapinduzi.
  • Kufuatilia hali ya kisiasa katika nchi jirani na nchi nyinginezo duniani.
  • Kufuatilia maendeleo ya Kamati za Urafiki na mshikamano kati ya Watanzania na wananchi wa nchi rafiki.
  • Kushughulikia masuala ya Itifaki ndani ya Chama.
Albamu