AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


VIJANA NENDENI HIJJA-DK. MWINYI

alternative

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewasisitiza vijana wa Kiislamu kwenda kufanya ibada ya Hijja pale fursa zinapotokea.

Alhaj Dk. Mwinyi ameeleza hayo leo wakati alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya Sala ya Ijumaa huko Masjid Mazrui, Mombasa Zanzibar.

Katika salamu zake hizo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa vijana wana nafasi nzuri kwa uwezo wao ama kupata msaada kutoka kwa Waumini wengine kwenda kuhiji na kamwe wasiziache fursa hizo ili waweza kutimiza nguzo ya tano ya Uislamu.

Hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi aliendelea kueleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Mfuko wa Hijja ili uweze kuwasaidia wasio na uwezo, kuweka fedha kidogo kidogo pamoja na kutoa fursa kwa wenye uwezo kuwasaidia wasio na uwezo kupitia Mfuko huo.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba Serikali itahakikisha inalifanyia kazi suala hilo ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha Waislamu wenye uwezo kuwasaidia Waislamu wenzao katika kutekeleza ibada hiyo.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alieleza umuhimu wa kuendeleza na kudumisha amani na umoja ndani na nje ya nchi na kuwataka wananchi kuienzi amani na umoja walionao nchini.

Alieleza kuwa maendeleo na shughuli nyengine za kuendeleza maisha zikiwemo ibada haziwezi kufanyika pindipo amani itakosekana.

Halikadhalika, Alhaj Dk. Mwinyi, aliwanasihi wananchi na kueleza kwamba  wanawajibu wa kudumisha amani iliyopo, licha ya kuwepo tofauti zao ambazo haziwezi kupelekea kukosekana kwa amani.

Akieleza suala zima la subira, Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba kwa upande wa Zanzibar juhudi za makusudi zimechukuliwa katika kuhakikisha amani inadumishwa ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha wananchi kupitia vyama vyao vya siasa na hatimae kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi aliwasisitiza viongozi wa dini, siasa pamoja na wananchi wote wasichoke kuhubiri amani na umoja uliopo kwa manufaa ya wananchi wote.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi aliwataka waumini wote wa dini ya Kiislamu kuyafuata na kuyafanyia kazi mafundisho ya Hijja kwa wale waliokwenda Makka na hata wale ambao hawakupata fursa ya kwenda kufanya ibada hiyo.

Nae Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Mfaume kwa upande wake alieleza msisitizo wa kuimarisha amani ambao amekuwa akiutoa Alhaj Dk. Mwinyi katika hotuba zake na kueleza kwamba ni miongoni mwa mafunzo ya Hijja.

Pamoja na hayo, alieleza haja kwa Waislamu wenye uwezo hapa nchini kuwasaidia wenzao wasio na uwezo kwenda kufanya ibada hiyo kama wanavyofanya Waislamu wengine katika baadhi ya nchi duniani huku akieleza umhimu kwa vijana wa Kiislamu kwenda Makka kufanya ibada hiyo.

Mapema akitoa hotuba ya Sala ya Ijumaa, Sheikh Twalib Juma Ali alieleza mafunzo ya Hijja na kusisitiza umuhimu kwa Waislamu waliokwenda Hijja kuyafanyia kazi.

Sheikh Twalib aliwanasihi waumini wa dini ya Kiislamu kuimarisha ibada na kuyaendeleza mafunzo ya Hijja katika maisha yote ya kila siku.

Habari Nyingine
Albamu