AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


DK. MWINYI AMALIZA ZIARA YAKE MKOA MJINI MAGHARIBI

alternative

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inayajenga wenyewe masoko ya Jumbi, Mwanakwerekwe na Chuini kupitia Jeshi a Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU).

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti katika muendelezo wa ziara yake katika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja ambayo leo imefikia tamati.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua uwamuzi huo baada ya Wawekezaji binafsi kushindwa kujenga masoko hayo.

Alisisitiza kuwa ujenzi huo utafanyika hivi karibuni na kukitaka kikosi cha (JKU), kisije kumuangusha kwani azma yake hivi sasa ni kukipa miradi kadhaa ya ujenzi kikosi hicho baada ya kuonesha umahiri mkubwa na nidhamu katika utendaji wao wa kazi.

Rais Dk. Mwinyi alikipongeza kikosi cha (JKU) na kueleza jinsi alivyoridhika na utendaji kazi wa kikosi hicho kwa wakati huku akiahidi kukipa kazi ya ujenzi wa skuli ya sekondari ya Mtopepo ambayo mkandarasi wake alimsimamisha hapo majuzi huku akitaka pale ajira zitakapoanza vijana wote waliojitolea kupitia kikosi hicho waajiriwe mwanzo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Hospitali ya Mkoa huko Lumumba yenye ghorofa sita, alieleza azma ya Serikali ya kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kutekeleza ahadi zake kwa vitendo sambamba na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Rais Dk.Mwinyi alieleza kwamba hivi sasa Serikali anayoiongoza inakwenda katika hatua mpya kwenye sekta ya afya huku akiahidi mazingira na maslahi mazuri ya wafanyakazi wa sekta hiyo pamoja na wengine wa sekta ya umma.

Aliahidi kuwepo kwa hospitali za Mikoa katika Mikoa yote ya Unguja na Pemba ambazo zitakuwa zikitoa huduma za kisasa.

Nao uongozi wa Wizara ya afya ulimpongeza Rais Dk. Miwnyi kwa juhudi zake hizo na kuwaomba wananchi waendelee kumuunga mkono kwani amekusudia kuiletea maendeleo endelevu Zanzibar.

Akiwa katika eneo la Wajasiriamali maara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya Wajasiriamali wa kusarifu mbao alisema kuwa Serikali imeamua kwa makusudi kwuawekea mazingira mazuri wajasiriamali ili waweze kufanya shughuli zao vizuri ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Alisema kwamba wakati umefika Zanzibar iwe na maeneo maalum kwa ajili ya biadhaa maalum ikiwa kwa lengo la kuuweka mji katika hali ya usafi pamoja na kuwarahisishia wananchi kujua mahala maalum pakwenda kununua bidhaa wanazozitaka.

Alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga fedha maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya michezo na kuliahidi Jimbo la Kwamtipura nalo kufaidika na fedha hizo. Pia, Rais Dk. Mwinyi alikagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya inayoendelea na ujenzi huko Chumbuni.

Mapema mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa skuli ya msingi ya ghorofa mbili huko katika eneo la Bint Hamrani alieleza azma ya Serikali ya kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa skuli za kisasa ili kupunguza idadi ya watoto madarasini.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa soko la samaki liliopo Malindi na baadae aligawa boti za uvuvi pamoja na boti kwa ajili ya wakulima wa mwani pamoja na kutoa zawadi kwa washindi wa mashindano ya madau.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba ndoto za uchumi wa buluu zinaanza kutekelezeka na kuyataja mambo makubwa matano yanayoimarisha sekta hiyo yakiwemo zana, soko, uhifadhi wa samaki, bandari maalum za uvuvi pamoja na viwanda.

Rais Dk. Mwinyi alieleza azma ya Serikali ya kutoa boti 577 kwa ajili wa wavuvi wa Zanzibar pamoja na hatua za kujenga masoko zaidi huku akieleza hatua za ujenzi wa kiwanda cha mwani huko Pemba na baadae kujengwa hapa Unguja.

Alisema kuwa Serikali imewakabidhi benki ya CRDB kutoa mikopo kwa wajasiriamali kwa kutambua kwamba wana uzoefu mkubwa huku akieleza jinsi Serikali ilivyobeba riba katika mikopo ya fedha kwa wajasiriamali.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliweka jiwe la msingi katika eneo la maduka la Darajani Bazaar na kusisitiza kuwa mara baada ya kukamilika wka ujenzi huo watakaowekwa kufanya biashara ni wale waliokuwepo awali na baada ya hapo ndio watapewa wafanyabiashara wengine.

Alieleza kwamba Serikali tayari imeshawawekea mazingira mazuri wajasiriamali wakiwemo wafanyabiashara huku akitumia fursa hiyo kukipongeza chama cha CCM kwa kukubali kubadilisha eneo hilo na kuekeza.

 

Habari Nyingine
Albamu