AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,amesema Chama Cha Mapinduzi hakitofanya upendeleo wa kutoa nafasi za kugombea uongozi kwa kigezo cha fedha na utajiri bali kitaweka mbele maslahi ya wanachama wote bila kujali hali zao za maisha.

alternative

Kauli hiyo ametoa wakati akiwahutubia viongozi na wanachama wa CCM katika Mkutano Mkuu Maalum wa Jimbo la Pangawe huko Wilaya ya Dimani Kichama Unguja.

Dkt.Dimwa,alisema kila mwanachama ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa hivyo ni lazima waondoshe dhana iliyojengeka siku za hivi karibuni kuwa wenye haki ya kugombea na kupata nafasi za uongozi ni watu wenye fedha na matajiri wakati Chama hicho kimetokana na wakwezi,wakulima na wafanyakazi.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo Dkt.Dimwa,alisema CCM itaendelea kusimamia kikamilifu misingi ya usawa,haki,uhuru na demokrasia pana ndani na nje ya Chama ili kutoa nafasi ya wanachama kunufaika na fursa mbalimbali zinazipatikana ndani ya Chama hicho.

“Wapo baadhi ya watu kila ikikaribia wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Dola wanawahadaa kwa fedha na vitu vya thamani wanachama wetu ili wawachague na wakisha pata uongozi wanapandisha mabega na wanajisifu kuwa tulipata Ubunge,Uwakilishi na Udiwani kwa sababu ya fedha zetu hivyo mtuache turejeshe fedha zetu kwanza maendeleo baadae.

Awamu hii watu wa aina hiyo mkiwaleta basi mjue hawatovuka kwani kigezo chetu ni kuangalia sifa za msingi za mgombea na tukiridhika naye hata akiwa mnyonge na maskini huyo huyo ndo tutaenda naye.”,alisema na kuongeza kuwa CCM sio mali ya matajiri bali ipo kwa manufaa ya wananchi wote.

Kupitia hotuba yake Naibu Katibu huyo,aliwapongeza Mwakilishi,Mbunge na Madiwani wa Jimbo la Pangawe kwa kazi nzuri wanayofanya ya kushirikiana katika kutatua changamoto za wananchi wa jimbo hilo ikiwemo zoezi la kutoa sadaka ya futari kwa wananchi wenye mahitaji ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Pamoja na hayo amewapongeza waumini wa dini ya kikiristo kwa kuathimisha siku kuu ya Pasaka pamoja kuwasihi waumini wa dini ya kiislamu kuendelea kufanya ibada kwa wingi,kujikataza na maasi na kutoa sadaka ili funga zao katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani zikubaliwe na Mwenyezi Mungu.

Aliwasihi wanachama hao kuendelea kuthamini na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi kwa kutekeleza llani ya CCM ya mwaka 2020/2025 kwa ufanisi mkubwa.

Naibu Katibu mkuu huyo Dkt.Dimwa, alizindua rasmi zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya kisasa kwa Mabalozi wa mashina wa CCM pamoja na kuwapatia posho la shilingi 20,000 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Hussein  Mwinyi litakalofanyika katika majimbo yote ya Zanzibar.

Pia Dkt.Dimwa, aligawa sadaka ya futari kwa niaba ya uongozi wa jimbo  zikiwemo sukari,mchele,mafuta ya kula na unga wa ngano kwa makundi mbalimbali ya Watu wenye mahitaji Maalum,Wazee,Wajane,Masheha na Mabalozi wa Jimbo la hilo.

Akizungumza Mwakilishi wa Jimbo la Pangawe  Ali Suleiman Mrembo,amesema lengo la Mkutano huo Maalum wa Jimbo ni viongozi hao kurejesha shukrani kwa wanachama wa CCM wa ngazi mbalimbali kutokana na kazi nzuri waliyofanya ya kuvuka malengo katika awamu ya kwanza ya zoezi la uhakiki wa Daftari la kudumu la uandikishaji wa wapiga kura.

Naye Mbunge wa Jimbo la Pangawe Haji Amour Haji,amesema mafanikio yaliyofikiwa ndani ya jimbo hilo yametokana na dhamira ya dhati ya viongozi hao ya kuleta maendeleo kwa kila mwananchi inayochechewa na ushirikiano kutoka kwa Wanaccm na wananchi wenyewe.

alternative alternative alternative
Habari Nyingine
Albamu