AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuendeleza fursa za kuajiri walimu wengi zaidi wa fani zote ili kuondosha changamoto ya walimu Zanzibar.

alternative

Dk. Mwinyi ametoa agizo hilo wakati wa ufunguzi wa Skuli ya Msingi ya Hamid Ameir iliopo Donge Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamrashamra za maadhimisho ya sherehe za kutimiza miaka 60 ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar.

Alisema, kada ya ualimu ni fani muhimu kuliko zote kwenye sekta za maendeleo, hivyo ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuboresha mazingira bora ya Elimu kwa kuweka sawa mazingira wezeshi ya sekta hiyo pamoja na kuimarisha maslahi ya walimu.

Pia, Rais Dk. Mwinyi ameahidi kuongeza uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya elimu kwa kuipa kipaumbele bajeti ijayo ya sekta hiyo ili kuimarisha mazingira bora kutoka ngazi ya maandalizi, msingi hadi Sekondari na kuimarishwa vituo vya amali pamoja na kujenga dahalia za kisasa kabla ya mwaka 2025.

Vilevile, Rais Dk. Mwinyi alisema, nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga ghorofa hadi skuli za maandalizi na dahalia ambayo inakwenda kutimia kama ilivyokamilisha skuli ya msingi ya Hamid Ameir kwa kuwa na madara mengi yaliyopindukia idadi, kuwa na wanafunzi chini ya idadi ya 45 pia inashuhudiwa kuwa skuli ya kwanza kuwa na mkondo mmoja tuu.

Alieleza hatua hiyo inatarajiwa kuzaa matunda bora ya matokeo mazuri kwenye kuongeza kasi ya ufaulu mzuri wa wanafunzi.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo, kuwasihi wazazi na walezi kuzitumia skuli hizo kwa kuandikisha wanafunzi wengi zaidi pamoja na kuiasa jamii kuyatunza na kuyaenzi majengo hayo ili yadumu muda mrefu.

Akizungumzia miaka 60 ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alisifu hatua za waasisi wa Muungano huo na wote waliojitolea kuutunza na kuuenzi na kueleza kuwa Muungano wa mfano Afrika uliodumu muda mrefu sana.

Naye, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdul Gulam Hussein alisifu jitihada za Rais Dk. Mwinyi kwa uwekezaji mkubwa aliowekeza Wizara hiyo.

Alisema, Wizara hiyo tayari imekamilisha magorofa 20 ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Dk. Mwinyi na kuahidi kumalizia ujenzi wa skuli za ghorofa kwa majimbo yote ya Unguja na Pemba kama ambavyo Wizara hiyo imekamilisha kwa baadhi ya majimbo zikiwemo skuli tano za Mkokotoni, Bumbwini, Tumbatu na Gamba zinazotarajiwa kukamilika mwezi wa tisa mwaka huu.

Aidha, alieleza Wizara ya Elimu na Mafuzo ya Amali tayari imeingiza makontena 60 ya vifaa vya skuli mpya zikiwemo meza, komputa, projekta, mashine za fotokopi, vitanda kwa dahalia zilizokamilika sambamba na kukamilisha ujenzi wa Dahali tatu kubwa kwa mkoa wa Kaskazini Unguja kwa maeneo ya Donge, Gambana Bumbwini.

Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo la Donge ambae pia ni Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Dk. Khalid Salum Muhamed alimshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa kufanikiwa kupeleka miradi mingi jimboni humo kiliwemo soko la kisasa Donge Mtambile, ujenzi wa Daraja kubwa Donge Chechele, kuboresha barabara za vijini pamoja na kuondosha msongamano mkubwa wa wanafunzi kwa ujenzi wa skuli za kisasa za Ghorofa.

Katibu mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdalla alisema ujenzi wa Skuli ya msingi ghorofa mbili ya Hamid Ameir uligharimu shilingi bilioni 4.5, umejumuisha madarasa 26, ofisi za walimu, ofisi ya mwalimu mkuu, vyoo, maktaba, maabara, chumba cha kompyuta na stoo.

Alisema, skuli hiyo ina wanafunzi 1173 kwa wastani wa wanafunzi 50, na sasa itakuwa na mkondo mmoja kwa wastani wa wanafunzi 41 kila darasa moja.

Akizungmza kwenye ghafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rashid Hadid Rashid amepongeza juhudi za Rais Dk. Mwinyi kwa kuinua Sekta ya Elimu Zanzibar.

Alisema, Mkoa wa Kaskazini umebahatika majengo matano ya ghorofa ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, yakiwemo majengo ya ghorofa kwa Skuli za Misufini na Makoba kwa Bumbwini Wilaya ya Kaskazini A, Skuli ya Donge, Mkokotoni na Tumbatu kisiwani.

Pia, Hadid alipongeza jitihada za Dk. Mwinyi kusambaza vituo vya sayansi (Hubs) kwa mitaala ya sayansi kwa vituo vya Fukuchani, Mahonda, Kitope, Donge, Bumbwini na Tumbatu pamoja na ujenzi dahalia kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita na ujenzi wa dahalia ya ghorofa maeneo ya Gamba.

Akitoa salamu kutoka Chama Cha Mapinduzi, Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Idara ya Itikadi Uenezi na mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis alisema, Ilani ya Chama hicho ya 2020 – 2025 ndio mkataba baina ya Serikali na wananchi kwa kutekeleza had izote kwao.

Alisema ilani hiyo imezungumzia masuala ya elimu kutoka maandalizi hadi vyuo vikuu ambapo kwasasa imepitiliza malengo ya Ilani hiyo kwa kuongeza ufaulu na kujenga madarasa maradufu hasa kwa skuli za vipawa vya juu zikiwemo Lumumba kwa Unguja na Fidel kasro kwa Pemba.

alternative alternative alternative
Habari Nyingine
Albamu