AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema uamuzi wa kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK) ulizingatia kutanguliza mbele usalama wa maisha ya watu kuliko maslahi ya vyama vya siasa.

alternative

Balozi Dk. Nchimbi ameongeza kusema kuwa uwepo wa Serikali hiyo Zanzibar umeondoa hali ya siasa za chuki na uhasama mkubwa uliokuwepo kabla ya kufikiwa kwa uamuzi wa kuundwa kwake, huku akisisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kutimiza wajibu wake wa kuongoza kwa misingi ya haki na uwajibikaji ili kudumisha umoja na utulivu nchini.

Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Nchimbi amesema hayo alipokuwa akizungumza na Wazee wa Mikoa minne ya CCM Kichama Unguja ikiwa ni siku ya pili akiwa kwenye ziara ya kikazi, akitokea Pemba ambako pia alifanya mazungumzo na mashauriano na Wazee wa Pemba.

“Binafsi nikimsikia mtu anazungumzia kutaka kujitoa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa(SUK), simwelewi huyo mtu hata kidogo.

Kwa sababu Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikuwa kwa ajili ya usalama wa maisha ya watu, usalama wa Wazanzibar, usalama wa Watanzania. Maisha ya watu ni muhimu sana kuliko kitu chochote kwanza. Tuliweka mbele maslahi ya nchi, utulivu na umoja wetu, si vyama vya siasa.

“Mnakumbuka wakati fulani nikiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kila siku nenda rudi kwa helkopita kuja Zanzibar. Tulikuwa tunahangaika kuondosha uhasama na chuki. Najua kuna wakati wenzetu wanapata gadhabu na kuzungumza kwa jazba lakini tuendelee kuwavumilia.

Sisi Wana CCM tusiende huko hata kidogo. Sisi ndiyo Chama tawala Sisi ni walezi, Mlezi hasusi, Tusiache wajibu wetu wa kulea hata kidogo na kwamba Mtoto ndiye anasusa. na katika hili naomba sana wazee wote wa Zanzibar na Tanzania, mniunge mkono,” amesema Balozi Dk. Nchimbi.

Aidha, Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Nchimbi pia amesisitiza msimamo wa CCM kuendeleza kutimiza wajibu wa kipekee wa kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na misingi yake, akisema kuwa ndiyo yaliyowaweka watu wote kuwa sawa mbele ya sheria na kuondoa kila aina ya ubaguzi, ukiwemo wa matabaka, rangi na hali ya mtu.

“Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yameondoa matabaka yakaleta utu, sote tunaunganishwa na utu wetu, tunao wajibu wa kipekee kuhakikisha tunaendelea kulinda misingi ya Mapinduzi.

Tuko tayari kuendelea kuyalinda hakuna umbo au rangi au hali inampatia haki zaidi mtu mwingine kuliko mwingine na ukifanya ubaguzi wa namna hiyo wewe ni kaburu tena ukaburu hauna rangi”,alieleza Dkt.Nchimbi.

Akiwakaribisha katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu Balozi Dk. Nchimbi aliwaambia Wazee wa Zanzibar kuwa wao ni mashahidi jinsi ambavyo awamu tofauti za Serikali za CCM, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimefanya kazi kubwa ya maendeleo ya watu.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,alisema CCM inajivunia kwa kuwa na hazina ya Wazee wenye uzalendo,busara,hekima na uwezo wa kushauri mambo mambo mbalimbali yenye manufaa kwa maendeleo ya Chama na Serikali zake kwa ujumla.

Dkt.Dimwa, alieleza kuwa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la Disemba 2022 ibara ya 124  inafafanua kuwa kutakuwa na Baraza la Wazee wanaotokana na CCM katika kila ngazi ya Uongozi isipokuwa ngazi ya Taifa. Wajumbe wa mabaraza hayo watakuwa Wazee wote (kuanzia miaka 60) wanaokubali imani, malengo na madhumuni ya CCM.

Mapema Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar Bi.Hadija Jabir,aliwasihi Wazee hao kuendeleza utamaduni wa kukosoa,kushauri na kutoa maoni ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi pale wanapoona kuna mambo yanaenda kinyume na misingi ya kuanzishwa kwa Chama hicho.

alternative alternative
Habari Nyingine
Albamu