AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China katika mambo mbali ya Kimaendeleo ikiwemo Sekta ya Uchumi wa Buluu, Miundombinu, Mafuta na gesi.

alternative

Ameyasema hayo wakati  alipofanya mazungumzo na Gavana wa jimbo la JIANGSU nchini China  Bwana XU KUNLIN na ujumbe wake waliofika ofisini kwake Vuga kwa ajili ya kufanya mazungumzo kufuatia kutimia kwa miaka 60 ya ushirikiano wa China na Zanzibar katika sekta ya Afya.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipa kipaumbele Sekta ya uchumi wa Buluu ambayo imekuwa ikitoa fursa mbali mbali za ajira kwa wananchi hivyo amemtaka Gavana huyo kuendeleza mashirikiano katika sekta hio pamoja na Sekta nyengine ikiwemo Afya, Miundombinu, Utalii, Mafuta na Gesi.

Mhe. Hemed amesema wakati China na Zanzibar inatimiza miaka 60 ya ushirikiano katika Sekta mbali mbali ikiwemo sekta  ya Afya, Zanzibar inajivunia kuendelea  kupokea madaktari wa kada mbali mbali kutoka China ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii na kutoa msaada mkubwa katika masuala ya Kitabibu.

Sambamba na hayo,   Makamu wa Pili wa Zanzibar amemuhakikishia Gavana XU KUNLIN kuwa Zanzibar itaendeleza ushirikiano uliopo na Serikali ya watu wa China na kuwataka kuendelea kuwekeza Zanzibar katika maeneo mbali mbali ya kiuchumi na kimaendeleo.

Kwa upande wake Gavana wa Jimbo la JIANGSU nchini china Bwana XU KUNLIN ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano  wa muda mrefu kupitia Nyanja mbali mbali ikiwemo za elimu na afya .

Amesema Jimbo la JIANGSU limekuwa likipiga hatua katika mambo mbali mbali yakiwemo masuala ya  Uchumi hivyo  wako tayari kushirikiana na Zanzibar katika eneo hilo ili kuhakikisha inazidi kupiga hatua kwa maslahi mapana ya wananchi wa pande zote mbili.

Bwana XU KUNLIN amesema katika sekta ya Afya China itahakikisha inaendeleza ushirikiano na  Zanzibar katika suala la Teknolojia katika kukinga na kutibu maradhi mbali mbali sambamba na kuwapatia Taaluma na kuwajengea uzoefu watendaji wa Wizara ya Afya .

Nae Waziri wa Afya Mhe. Nassor Ahmed Mazurui ameishukuru Serikali ya watu wa  China kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar hasa katika sekta ya Afya kwa kuleta madaktari bingwa kuja Zanzibar kwa kutoa msaada wa kitabibu kila mwaka na kuwajengea uwezo madaktari wazawa .

Mhe. Mazurui amesema Miaka 60 ya ushirikiano katika sekta ya Afya kwa Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China umeleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika sekta ya hio ikiwemo kuboreshwa kwa  upatikanaji wa huduma kuanzia Vituo vya Afya hadi Hospitali ya Rufaa zilizopo nchini.

alternative
Habari Nyingine
Albamu