AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


DK. MWINYI AMEFUNGUA SKULI YA KIDONGOCHEKUNDU MSINGI

alternative

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema miaka 59 ya Muungano wa Tanzania imeleta Mapinduzi makubwa kwenye sekta ya Elimu kwa pande zote ikiwemo kuboresha miundombinu ya majengo ya kisasa na huduma zenye ubora katika kutoa ufaulu mzuri kwa wanafunzi.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye sherehe za ufunguzi wa Skuli ya msingi ya kisasa Kidongochekundu iliopo kwenye jimbo la Jang’ombe, Wilaya ya Mjini ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Muungano wa Tanzania.

Alisema, Zanzibar kwasasa inastahiki kuwa na skuli za msingi za ghorofa zenye ubora wa hali ya juu ili kuendana na hadhi ya miaka 59 ya Muungano wa Tanzania ambapo Serikali zote mbili ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeshuhudia ongozeko kubwa la taasisi nyingi za elimu na wanafunzi wengi.

Alisema, kabla ya Muungano wa Tanzania, sekta ya elimu ilikua na wanafunzi 25, 000 na sasa idadi imeongezeka kufikia 570,000.

Akizungumzia miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali ina mpango wa kuongeza madarasa 1000 yenye miundombinu na vifaa vya kisasa zikiwemo maabara, vyumba vya kompyuta, maktaba, vyoo vya kisasa na ofisi za walimu pamoja na kufungua miradi mikubwa zaidi ya maendeleo.

Alisema mabadiliko ya elimu Zanzibar yatafikiwa kwa kuwa na ujenzi imara wa miundominu ya majengo ya kisasa yatakayochukua wanafunzi wachache kwenye madarasa, vifaa vya kisasa na mazingira mazuri ya kufundisha na kujinza. 

Rais Dk. Mwinyi aliongeza skuli ya Kidongochekundu Msingi ni miongoni mwa mfano hai wa skuli zote za msingi anazotaka kuzijenga Zanzibar hadi kufikia Januari, 2025 pamoja na kukamilisha miradi mengine mikubwa ya maendeleo ili kuendana na hadhi ya miaka ya Mapinduzi ya Zanzibar na miaka 59 ya Muungano wa Tanzania.

“Skuli hii ni mfano wa skuli zetu za msingi nnazotaka ziwe nchini, skuli za ghorofa ambazo ndani yake mna maabara za sayansi, maktaba, vyumba vya kompyuta na madarasa wanafunzi wetu wasiozidi 45” alielekeza Dk. Mwinyi

Alisema serikali itafanya kila jitihada kuhakikisha Zanzibar inapata madarasa ya kutosha, nyenzo bora za kusomea ikiwemo kufanikisha skuli kuwa na mkondo mmoja badala ya miwili kama awali. Aidha, aliwataka watendaji wa wizara ya elimu kuhakikisha skuli inatoa huduma zinazoendana na hadhi yake kwa kutoa ufaulu mzuri kwa wanafunzi. 

Naye, Waziri wa Elimu  na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa alisema ujenzi wa skuli hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya 2020/2025 ambapo  serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliahidi  kujenga miradi malimbali ya maendeleo.

Alieleza Wizara ya Elimu imepiga hatua kubwa katika kukamilisha miradi yote iliyopanga na kwamba imeakisi dhima ya miaka 59 ya Muungano wa Tanzania. 

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Khamis Said alisema ujenzi wa skuli hiyo umegharimu shilingi bilioni 4.466 ambao umejumuisha Maktaba, Maabara, chumba cha kompyuta, ofisi ya mwalimu kuu, ofisi ya msaidizi mwalimu mkuu, ofisi tatu za walimu, chumba cha kusalia, vyoo 25 , viti na meza 1305 kwaajili ya wanafunzi wote.

Skuli ya Msingi Kidongochekundu ni miongoni mwa skuli mpya  zilizojengwa na Serikali ya awamu ya nane kwa fedha za ahuweni ya uviko 19 Zanzibar, kwa Unguja na Pemba. 

Habari Nyingine
Albamu