AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


Serikali yaja na Helikopta kukabiliana na Majanga ya Moto

alternative

Serikali yaja na Helikopta kukabiliana na Majanga ya Moto

Serikali imedhamiria kufanya maboresho makubwa katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ikiwa ni juhudi za kupambana na athari za majanga pindi zitokeapo ajali mbalimbali ikiwemo ajali ya moto ili kuweza kuokoa mali na maisha.Maboresho hayo yanajumuisha ununuzi wa magari ya kuzimia moto yasiyopungua 150,magari 20 ya Kubebea Wagonjwa, Boti za Kisasa 25 za Uokozi  na Helikopta Moja  Maalumu  ya Uokozi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni wakati akizungumza katika Mkutano wa Kuwajengea uwezo Wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara na Makatibu Tawala, ulioandaliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI), katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani ambapo pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Daniel Chongolo.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inakwenda kufanya uwekezaji mkubwa katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambapo tutashuhudia magari ya Zimamoto na Uokoaji yasiyopungua 150 yakimwagika, Boti Maalumu za Uokozi zisizopungua 25, Gari Maalumu za Kubebea majeruhi (Ambulance) zisizopungua 20, na Helikopta, lengo ikiwa kuokoa mali na Maisha ya Watanzania pindi yanapotokea majanga” alisema Mhandisi Masauni

Waziri Masauni amewaomba pia Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kunakuwepo vituo vya kuchotea maji ambayo yatatumika pindi yatokeapo majanga ya moto huku akitaja maeneo mengine ya vipaumbele kwa Jeshi la Zimamoto kuwa ni kuimarisha vitendea kazi vya Zimamoto na Uokoaji, Ujenzi wa Vituo vya Zimamoto  pamoja na Nyumba za Makazi ya Askari wa Jeshi hilo na kuwasiliana na Mamlaka za Maji katika mikoa mbalimbali nchini ili kuweza kusimika mabomba ya kuzimia moto(fire hydrants) huku pia serikali ikitenga kiasi cha shilingi milioni 120 kwa ajili ya ukarabati wa vituo vibovu.

“Serikali imeendelea  na Ujenzi wa Vituo vya Zimamoto na Uokoaji katika maeneo mbalimbali nchini lengo ikiwa ni kuboresha huduma za uokoaji katika maeneo hayo na katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 jumla ya Shilingi Bilioni 2 zimetengwa kwa ajili ya Ujenzi na Uendeshaji wa Vituo Saba vya Zimamoto na Uokoaji katika mikoa ya Songwe, Simiyu, Manyara, Kagera, Katavi, Geita na Njombe, vilevile Shilingi Milioni 400 zimetengwa kwa ajili ya Ukarabati wa Nyumba 10 za Makazi ya Askari katika mikoa ya Arusha, Morogoro na Iringa”

alternative alternative alternative alternative
Habari Nyingine
Albamu