AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


TUENDELEE KUUNGANA KUPIGA VITA UDHALILISHAJI

alternative

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameitaka Jamii kuungana katika kuendeleza vita dhidi ya udhalilishaji Nchini.

Mhe. Hemed ametoa wito huo katika Maadhimisho ya Siku ya Ustawi wa Jamii Duniani yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Shekh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Amesema Serikali ya Awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi inaendelea na juhudi mbali mbali ikiwemo uanzishwaji wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Jinsia, wazee na watoto ili kuhakikisha janga la udhalilishaji linamaliza katika Jamii ya wazanzibari.

Amesema mashirikiano ya pamoja kwa Maafisa ustawi, watendaji wote Serikalini na Jamii kwa ujumla yatasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupata Jamii iliyo bora.

Aidha Mhe. Hemed amezitaka Taasisi zinazosimamia masuala ya udhalilishaji kuacha muhali na kuchukua hatua stahiki kisheria bila ya kumuonea mtu yoyote.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza kusimamia misingi ya sheria katika kujenga jamii ya wazanzibari yenye ustawi ulio bora.

Pamoja na hayo Mhe. Hemed amekemea tabia ya baadhi ya watu na Asasi za kiraiya kuwatumia mayatima na watu wenye ulemavu  kuwa ni mradi na kitega uchumi cha kuwapatia kipato binafsi na kueleza kuwa hiyo  pia ni aina ya udhalilishaji katika jamii.

Amesema ni mila, silka na desturi ya Kizanzibari mayatima kulelewa ndani ya Familia zao ili kupata makuzi mema na yenye maadili.

Aidha Mhe. Hemed amesisitiza wazazi na walezi kutokimbia majukumu yao ya kulea watoto ili kuepuka kupata watoto wa mtaani waliokosa malezi ambao hupelekea kujiingiza katika matendo maovu ikiwemo udhalilishaji,  utumiaji wa Madawa ya kulevya na wizi.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma amemshkuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuona umuhimu wa kuimarisha ustawi wa Wazanzibari kwa vitendo na kuahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Serikali ili kufikia lengo la kuanzishwa Wizara hiyo.

Aidha ameahidi kuwa Wizara  itaendelea kukemea matendo yote ya udhalilishaji wa Kijinsia  ambayo yanaathiri jamii ya wazanzibar kimwili na kisaikolojia.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto Ndugu Abeida Rashid Abdalla ameeleza kuwa Wizara imeandaa Mipango mbali mbali ya kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ikiwemo kuanzisha Kliniki ya Sheria,  elimu na ushauri, pamoja na kuanzisha mafunzo ya malezi yatakayosaidia kupunguza utekelezaji wa watoto nchi.

Aidha ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanzisha masomo ya kada ya Ustawi wa Jamii ambapo tayari wahitimu mia saba (700) wameshamaliza mafunzo ambao wanasaidia kutoa elimu ili kuiweka jamii katika ustawi mzuri.

Habari Nyingine
Albamu