AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR IMEAHIDI KUSAIDIA VIKUNDI VYA KINA MAMA ILI VIWEZE KUPATA MIKOPO NA KUJIKWAMUA KIMAISHA

alternative

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo alipofanya mazungumzo na Uongozi wa Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) waliofika kujitambulisha Ofisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.

Mhe. Hemed ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amesema Serikali inatoa Mikopo ya gharama nafuu kwa vikundi vya wajasiriamali kwa lengo la kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuwaahidi kina mama kuwa Serikali inatoa kipaumbele kwa wanawake ili waondokane na utegemezi.

Mhe. Hemed ameeleza kuwa dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kutenga fedha kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali ni kuweza kuwasaidia wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa urahisi na kuweza kujikimu kimaisha.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameupongeza Uongozi wa UWT kwa kuandaa mpango kazi ambao umelenga kuiletea mabadiliko Jumuiya hiyo hasa mpango wa kuanzisha vitega uchumi kwa kila Mkoa hatua ambayo itasaidia Jumuiya hiyo kuacha utegemezi katika kuendesha shughuli za kila siku.

Amesema,  Chama Cha Mapinduzi kimeelekeza kuboresha vitega uchumi na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa Jumuiya zake ili kurahisisha  uendeshaji wa shughuli za Chama za kila siku.

Pamoja na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaletea maendeleo watanzania ndani ya kipindi cha muda mfupi.

Aidha Mhe. Hemed amewasihi viongozi hao kuwa wavumilivu na kutovunjika moyo kwa changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Tanzania  Bi. Zainab Shomari  amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa UWT imejipanga kufanya mabadiliko kwa kujiimarisha kimaendeleo kiutendaji, kisiasa na kiuchumi.

Aidha ameeleza kuwa Umoja wa Wanawake Tanzania umefurahishwa kwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga Hospital zenye huduma za Mama na Mtoto hatua ambayo itasaidia kumaliza changamoto ya usumbufu wa kina mama wanapofata huduma hizo na kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Habari Nyingine
Albamu