Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua jitihada mbali mbali katika kupinga na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto.
Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya Uzindiuzi wa Kitabu cha Taarifa za Kesi za udhalilishaji wa kijinsia kwa mwaka 2022 na 2023 katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil Kikwajuni jiijini Zanzibar.
Amesema Miongoni mwa juhudi zinazo chukuliwa na Serikali katika kupambana na udhalilishaji ni pamoja na kuweka sheria mbali mbali za kuwalinda Wanawake na watoto dhidi ya vitendo hivyo sambamba na kuanzisha Mahakama maalum ya kesi za Udhalilishaji kwa kila Mkoa kwa lengo la kuhakikisha utoaji wa maamuzi wa kesi hizo unakamilika ndani ya muda mfupi.
Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali imeanzisha kamati ya kuzuia vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia iliyopo chini ya Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka iliyoshirikisha wajumbe kutoka Taasisi za Serikali, Taasisi za Dini na Taasisi Binafsi kwa lengo la kuangalia mianya ya udhalilishaji kisekta kama vile hospitali, maskulini ,madrasa na sehemu za kitalii pamoja na maeneo mengine ili kuweza kudhibiti vitendo vya udhalilishaji katika maeneo hayo.
Mhe.Hemed amesema kuwa jitihada hizo za Serikali zimeanza kuzaa matunda kwa kupungua matukio ya udhalilishaji kutoka kesi 432 zilizoripotiwa mwaka 2022 hadi kufikia kesi 348 zilizoripotiwa kwa mwaka 2023 na kushuka hadi kufikia kesi 289 kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba 2024.
Aidha, Makamu wa Pili wa Rais ameiagiza kamati ya kuzuia udhalilishaji wa kijinsia kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya mianya iliyopo ambayo inapelekea makosa ya udhalilishaji wa kijinsia kutokea pamoja na kuwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika kupiga vita vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Sambamba na hayo amesema kuwa kama Taifa lazima tuungane kwa pamoja bila kujali cheo, rangi, dini au hadhi ya mtu ili kuwa na sauti ya pamoja itakayohakikisha makosa ya udhalilishaji hayapewi nafasi katika jamii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameendelea kutoa wito kwa Viongozi wa dini,wanasiasa na wananchi kwa ujumla kuendelea kutoa elimu kwa wafuasi wao juu ya kumuogopa Mwenyezi Mungu na kukemea vitendo vya udhalilishaji sambamab na jamii kuondoa muhali na kuacha tabia ya kuyanyamazia au kupuuza matukio ya udhalilishaji ili jamii iweze kubaki salama.
Nae Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee, Wanawake na Watoto Mhe. Riziki Pemba Juma amesema vitendo vya udhalilishaji bado vinaendela kufanyika ndani ya Visiwa vya Unguja na Pemba licha ya Takwimu kuonesha kupungua kwa matukio ya vitendo hivyo.
Mhe. Pembe amesema kesi nyingi za udhalilisha zimekuwa zikikosa kutolewa hukumu kutokana na upelelezi wa kesi hizo kuchukua muda mrefu kukamilika kutokana na muhali uliopo kwa wanananchi wa kutoa ushahidi jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa watuhumiwa kuachiwa huru na watendewa wa vitendo hivyo kubakiwa na maumivu ya muda mrefu katika mioyo yao.
Amesema ushirikiano wa pamoja unahitajuka katika kupambana na kupinga vitendo vya udhalilishaji kwa kuwa tayari kutoa ushahidi Mahakamani na kushirikiana na Taasisi husika katika kuhakikisha sheria inafuata mkondo wake na watuhumiwa wanahukumiwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Mhe. Mgeni Jailani Jecha amesema lengo la kufanyika kwa uzinduzi wa Kitabu hicho cha Taarifa za udhalilishaji wa kijinsia ni kuifanya jamii kujua uhalisia wa matukio ya vitendo vya udhalilishaji nchini.
Mhe. Jailani amesema Takwimu zinaonesha kuwa waathirika wakubwa wa vitendo vya udhalilishaji ni watoto wa kike na wa kiume walio chini ya umri wa miaka 14 ambapo kwa mwaka 2022 watoto wa kike 329 wamefanyiwa udhalilishaji wa kijinsia ambapo jitihada za Serikali, Taasisi binafsi na wadau wa kupambana na vitendo hivyo zimepelekea upungua kwa vitendo hivyo na kufikia 258 kwa mwaka 2023.
Amesema kuwa udhaifu wa ushahidi wa kesi za udhalilishaji umetajwa kuwa ndio changamoto kubwa inayozikabili Mahakama katikahi uendeshaji wa kesi hizo jambo ambalo linachangia watuhumiwa kutotiwa hatiani kutokana na kutokuwepo na ushahidi wa kutosheleza kumtia mtuhumiwa hatiani hivyo ameiomba jamii kutoa ushirikiano ili kufanikisha azma ya Serikali ya kutokomeza vitendo vya udhalilishaji Zanzibar.
Aidha amefahamisha kuwa Takwimu zinaonesha wafanyaji wakubwa wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ni majirani na ndugu wa karibu wanaoaminiwa na wahanga wa vitendo vitendo hivyo.