AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


DK.HUSSEIN ALI MWINYI AMEZINDUWA MRADI WA KUWAJENGEA UWEZO VIJANA ILI WAWEZE KUJIAJIRI NA KUAJIRIKA KATIKA SEKTA YA UCHUMI WA BULUU

alternative

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza dhamira yake ya kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu kupitia Wizara yake ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alieleza dhamira hiyo kwenye ufunguzi wa mradi wa kuwajengea uwezo vijana kwa lengo la kuwawezesha kujiajiri na kuajirika kwenye sekta ya uchumi wa buluu huko ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa ndege, Zanzibar.

Dk. Mwinyi alisema, Serikali inaendeleza jitihada mbali mbali kwa kuhakikisha inatoa elimu bora nchini katika kufikia dhamira hiyo kwa kuchukua hatua za kuboresha miundombinu ya skuli mpya ikiwemo ujenzi wa Skuli mpya za ghorofa kwa Unguja na Pemba na mafunzo kwa walimu. 

Hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi alieleza ni kuzipatia huduma muhimu skuli hizo ikiwemo, upatikanaji wa vifaa bora vya kufundishia na kujifunzia, matumizi bora ya TEHAMA na kuwapatia vijana ujuzi na maarifa utakao wawezesha kuyakabili maisha yao na kunyanyua uchumi wa nchi.

“Kama hatutowaandaa vijana wetu, wakawa weledi wa kujua wanachokifanya, hatutofikia dhamira yetu ya kuhakikisha watu wote wakiwemo vijana wanashiriki na kunufaika na Uchumi wa Buluu” aliasa Rais Dk. Mwinyi.

Dk. Mwinyi alitaja sehemu ya ujenzi wa mradi huo ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha kisasa cha Ubaharia na majengo utawala, ujenzi wa hosteli ya wanafunzi wa kike kwenye Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume yenye ukubwa wa ghorofa tatu na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 500 kwa wakati mmoja, ujenzi wa madarasa ya kusomea na karakana zinazohusiana na masomo ya mafuta na gesi.

Aliongeza ujenzi wa vyuo vya mafunzo ya amali na vifaa vyote vinavyohitajika kwa programu zitakazotolewa na vyuo hivyo ambavyo vinatarajiwa  kujengwa  kwenye  Wilaya za Mkoani (Chambani), Wilaya ya Micheweni (Tumbe Mashariki), Wilaya ya Kati (Jendele) na Wilaya ya Kaskazini B (Panga Tupu). 

Shughuli nyengine za mradi huo wa SEBEP, Rais Dk. Mwinyi alizitaja ni pamoja kuwajengea uwezo watendaji wa Taasisi zinzozoshiriki kwenye mradi huo kwa kuwapatia nafasi za kuongeza taaluma zao, ujenzi wa kituo cha kuwapa vijana mafunzo ya kuanzisha na kuendeleza biashara zao (incubation centre) na vifaa vyake eneo la Kizimbani Unguja, ambacho kitakuwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) na taasisi ya SMIDA imepewa jukumu la kuwapatia mafunzo mbalimbali vijana hao.

Rais Dk. Mwinyi alisema hatua hiyo inatoa nafasi kwa Vijana wa Zanzibar kupata fursa ya mafunzo ya amali na ufundi  wa fani mbali mbali zikiwemo zinazohusiana na Uchumi wa Buluu.

Pia alitoa wito kwa vijana kuitumia vyema fursa ya mradi huo kujipatia ujuzi ili wanufaike na soko la ajira kwenye sekta ya uchumi wa buluu kwa kuweza kujiari na kupata sifa za kuajiriwa.

Dk. Mwinyi alisema mradi huo utaongeza upatikanaji wa wafanyakazi wenye taaluma kwenye shughuli za Utalii ambayo ni Sekta kiongozi  katika uchumi wa Zanzibar pamoja na kuiwezesha Zanzibar kuzitumia vyema rasilimali zake za asili ikiwemo bahari, mafuta na gesi asilia katika kukuza pato la taifa na upatikanaji wa ajira kupitia sekta ya Uchumi wa Buluu.

Mradi wa kuwajengea uwezo vijana kwa lengo la kuwawezesha kujiajiri na kuajirika kwenye sekta ya uchumi wa buluu SEBEP unafadhiliwa kwa asilimia 90 na washirika wa maendeleo (AfDB) na asilimia 10 unafadhiliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, unatarajiwa kutumia dola za Marekani milioni 54 sawa na fedha za Tanzania shilingi bilioni 126.379.

alternative alternative alternative alternative alternative
Habari Nyingine
Albamu