AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewataka watanzania kuhimizana kila wakati juu ya kuitunza amani iliopo nchini kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.

alternative

Ameyasema hayo alipokuwa akisalimiana na waumini wa Dini ya kiislamu katika Masjid KAHFI uliopo MKELE KWA BIMTORO Wilaya ya Mjini mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Alhajj Hemed amesema ili Taifa lipige hatua kimaendeleo ni lazima kuwepo na Amani na Utulivu ndani ya nchi, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi wa Tanzania na muumini wa Dini ya kiislamu na dini nyengine kuhakikisha anaienzi na kuilinda Amani iliyopo nchini kwa faida ya vizazi vya sasa na baade pamoja na Taifa kwa ujumla.

Makamu wa pili amesema zipo nchi duniani hawawezi kujumuika pamoja katika  kufanya ibada kutokana na kutokuwepo kwa amani na utulivu ndani ya nchi zao hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anaitunza tunu ya amani iliyopo kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

Amesema ni lazima kujifunza kutoka kwa nchi za jiarani jinsi wanavyokosa amani kwa sasa jambo ambalo linapelekea kukosekana kwa maendeleo na kuwataka wananchi kutokubali kushawishiwa na baadhi ya watu wasioitakia mema nchi yetu hasa kipindi cha siasa.

Aidha Alhajj Hemed amewataka baadhi ya viongozi kuacha kutoa maneno ya uwongo na yauchochezi ambayo yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani iliyopo nchini na kuwataka kuihubiri amani wakati wote ili kupata maendeleo kwa maslahi ya wananchi wote.

Sambamba na hayo Alhajj Hemed ameendelea kuwakumbusha waumini wa Dini ya Kiislamu na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum wakiwemo mayatima, wajane na wazee wasiojiweza ili kuzidisha upendo baina yao.

Amesema ipo haja ya kuitumia misikiti kwa kuyatambua makundi haya muhimu ili kuweza kuyasaidia ikiwa ni njia moja wapo ya kudumisha upendo na ushirikiano na kuweka usawa wa kila mwannchi.

Mapema akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa, Maalim MUHITA ALI HASSAN   amewataka waumini wa dini ya Kiislam kujitathmini na kujiangalia upya katika kufanya ibada hasa katika kipindi hichi cha kuukaribisha mwaka mpya wa kiislamu siku chache zijazo.

Amesema kuwa uislamu umewataka waumini kuhimizana katika kufanya ibada pamoja na kuwa wamoja kwa kila kitu hasa katika kuipigania dini ya kiislamu  ili kuweza kufikia malengo ya kuletwa hapa duniani.

alternative
Habari Nyingine
Albamu