Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo na Wizara ya Utalii na Mambo ya kale itaendelea kuweka Mazingira bora ya michezo Visiwani Zanzibar na kuboresha vivutio vya Utalii ili kuweza kuitangaza Zanzibar kimataifa.
Ameyasema hayo kwa niaba ya Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi wakati wa kukabidhi zawadi kwa washiriki wa Tigo/Zantel Zanzibar International Marathon yaliyofanyika katika viwanja vya Forodhani jijini Zanzibar.
Amesema kwa kipindi kirefu Zanzibar imekuwa ikijikita katika utalii wa msimu ( seasonal tourisim) ambao umeisaidia Zanzibar kuvutia watalii wengi kutembelea katika maeneo ya kihistoria kama vile mji mkongwe na maeneo ya bahari ambapo jumla ya watalii laki sita na mia tatu(600,300) wametembembelea Zanzibar kwa mwaka 2024.
Makamu wa Pili wa Rais amesema kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa na eneo kubwa la bahari ambalo likitumika vizuri kwenye utalii Zanzibar itaweza kuongoza katika Ukanda wa Afrika katika utalii wa Michezo ya baharini sambamba na kuwataka wadau mbali mbali kujitokeza na kuiendeleza michezo ikiwemo michezo ya marathon, kuogelea, mbio za pikipiki za baharini na mashindano ya ngalawa ili kuitangaza Zanzibar kimataifa.
Sambamba na hayo Mhe.Hemed amesema Serikali imepanga kujenga uwanja mpya wa mpira wa miguu ambao utatumika katika mashindano ya Afcon 2027 pamoja na kuvifanyia ukarabati mkubwa viwanja vya New Amani Complex na Uwanja wa Gombani Stadium Pemba ili kuendana na viwango vya kimataifa na kuweza kuitangaza Zanzibar kupitia michezo na utalii.
Aidha amewataka wanamichezo na wananchi kwa ujumla kuendelea kulipa kodi kwa hiari kwa kudai risiti wanaponunua bidhaa na kwa upande wa wafanyabiashara kutoa risiti wanapofanya mauzo jambo litakalosaidia kuziba myanya ya upotevu wa mapato ya Serikali na kuweza kupiga hatua kimaendeleo.
Nae waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe.Mudrik Ramadhan Soraga ameipongeza Tigo/Zantel Zanzibar International Marathon kwa kuendelea kulitumia eneo la Ngome Kongwe kama ni kituo cha kuanzia mashindano hayo jambo ambalo linasaidia kuzidi kuutangaza Urithi huo wa Mji Mkongwe na Utalii kwa ujumla.
Amesema kufanyika kwa Mashindano haya yanatoa fursa kwa Mataifa mbali mbali kushiriki katika mashindano hayo na washiriki kupata nafasi ya kuvitembelea vivutio mbali mbali vya utalii vilivyopo Zanzibar na kuweza kuitangaza vyema Zanzibar wakati wanaporudi nchini mwao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tigo/Zantel Zanzibar International Marathon ndugu Hassan Mussa amesema wanampongeza Rais wa Zanzibar kwa kuboresha miundombinu ya Michezo kwa kuboresha na kujengwa viwanja vipya na vya kisasa vya michezo pamoja na barabara ambazo ni rafiki kwa wanariadha.
Amesema Tigo/zantel kwa kushirikiana na wadau wengine wa Zanzibar International Marathon wataendelea kuunga mkono juhudi za Mhe. Dkt.Mwinyi za kuimarisha Sekta ya michezo nchini ambapo ndani ya miaka kumi(10) ya uongozi wa Dkt Mwinyi wamejipanga kuyaboresha mashindano hayo ili yazidi kuwa kivutio kikubwa cha Utalii kwa wageni wanaingia Zanzibar.
Kwa upande wao Wadhamini wakuu wa mashindano hayo Tigo/ Zantel na Benki ya Eatu wa Zanzibar (PBZ) wamesema wataendelea kudhamini mashindano hayo na mashindano mengine ili kuiunga mkono serikali ya awamu ya Nane ( 8 ) sambamba na kuviendeleza vipaji vilivyopo nchini kupitia michezo mbali mbali.