AnuaniKisiwandui, Zanzibar
Simu(+255) 26 23 22965

Habari na Matukio Mbalimbali


SERIKALI INAFANYA JITIHADA KUBWA KUIMARISHA SEKTA YA AFYA - DK. MWINYI

alternative

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza jitihada kubwa iliyofanya ya kuimarisha sekta ya Afya nchini kwa kuongeza bajeti ya sekta hiyo na kujenga miundombinu ya kisasa ikiwemo ujenzi wa hospitali za Wilaya na Mkoa pamoja na kuzifanyia matengenezo makubwa hospitali na vituo vya afya vya Unguja na Pemba. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul – Wakili, Kikwajuni Wilaya ya mjini, kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani.

Alisema Serikali ya awamu ya nane kupitia Wizara ya Afya imeanza kuajiri wauguzi ili kupunguza changamoto ya uhaba wa watumishi hao na kuahidi kuendelea kufanya hivyo kwenye mwaka wa fedha ujao.

Pia Dk. Mwinyi alieleza, Serikali imeongeza nafasi za ajira kwa madaktari na watumishi wengine kwenye sekta hiyo pamoja na kuendeleza mpango wa mafunzo wa kuwajengea uwezo watumishi wake kwa lengo la kuwaongezea ufanisi.

Rais Dk. Mwinyi alieleza jitihada za Serikali kununua vifaa vya kisasa vya uchunguzi na tiba. 

Vilevile Dk. Mwinyi aliwakumbusha Wauguzi na Watumishi wa sekta ya afya kuendelea kuisaidia Serikali kwenye utekelezaji malengo yake ya kuwapatia huduma bora za afya wananchi wa Zanzibar bila ya kuwabagua ili kutekeleza Shabaha ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 katika huduma bora za afya na mipango mikuu ya sekta ya Afya nchini. 

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi aliwanasihi wauguzi hao kuendelea kuwa na moyo wa huruma, kutumia lugha nzuri na kufuata maadili ya taaluma yao wakati wote wanapowahudumia wagonjwa.

Aliwasihi wauguzi hao na wakunga, kushirikiana na kada nyengine za sekta hiyo ili kuimarisha huduma bora kwa wananchi.

“Ili kufanikisha utoaji wa huduma bora za afya, ushirikiano na kada nyengine ni muhimu na ni lazima, wakiwemo, madakatari, wafamasia, wachunguzi na wahudumu. Hivyo, hakikisheni mnaimarisha ushirikiano na kada hizo ili wananchi wetu wapate huduma zilizo na ubora unaotakiwa” alinasihi Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi, aliwataka viongozi wa Wizara ya Afya na wauguzi kuhakikisha wanafuatilia utekelezaji wa miongozo iliopo ili hadhi na heshima ya taaluma ya uuguzi iendelee kudumu kwa kufuata vitabu vya miongozo vilichotolewa na Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar, katika utekelezaji wa majukumu yao.

Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi aliwataka wauguzi hao kuongeza bidii kwa kufanya kazi kwa moyo, uzalendo na kujituma wakati Serikali inaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili kada yao.

Pia Dk. Mwinyi alitoa wito kwa wauguzi hao kutumia fursa za kujiendeleza kitaaluma ili kwenda sambamba na mabadiliko ya utoaji wa huduma za kisasa kwenye sekta ya afya. 

Kwa upande wa wauguzi hao, walimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba, kada ya uuguzi imetoa mchango mkubwa kwenye jamii ikiwemo kupunguza vifo vya watoto wachanga, kupunguza malaria, polio, kifua kikuu, kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na kupunguza maambukizi ya UVIKO 19.

Akisoma risala kwa niaba ya wauguzi wenziwe, Muuguzi Saida Kheir Hamad alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba, wauguzi wa Zanzibar waliiadhimisha siku hiyo kwa kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo kutoa elimu juu ya kujikinga na maradhi mbalimbali yanayoambukiza na yasiyoambukiza, elimu juu ya unyonyeshaji sahihi kwa watoto, uhamasishaji na utoaji huduma za uzazi wa mpango, chanjo kwa mama wajawazito na watoto, uchunguzi wa dalili za awali za saratani ya shingo ya mlango wa kizazi na matiti.

Chimbuko la Maadhimisho ya siku ya Wauguzi duniani, Mei 12 ya kila mwaka ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa muasisi wa huduma za uuguzi aitwae Florence Nightingale mwaka 1820 Itali, ambae historia inamueleza alitoa mchango mkubwa katika kada ya uuguzi pamoja na wauguzi wengine kote duniani. 

Kwa kuzingatia umuhimu wa kada ya uuguzi duniani, ndipo Shirika la kimataifa la wauguzi liliikatangaza tarehe 12 Mei ya kila mwaka kuwa Siku ya Wauguzi Duniani.

Habari Nyingine
Albamu