Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza Uongozi wa Mfuko wa hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kuwasimamia vyema wakandarasi na washauri elekezi wanaojenga miradi yao ili kuhakikisha wanamaliza kwa wakati uliopangwa na kwa kiwango cha hali ya juu
Ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi mbali mbali inayojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).
Mhe. Hemed amesema miradi yote ya kimaendelea inayojengwa na Serikali inadhamira ya kuwaondolea wanachi changamoto ya makaazi, kuwainua kichumi sambamba na kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo endelevu kwa maslahi ya vizazi vya sasa na baadae.
Mhe. Hemed amesema wakati umefika kwa wakandarasi wanaopewa dhamana ya kujenga miradi ya Serikali kuhakikisha wanaikamilisha kwa wakati uliopangwa na kushindwa kukamilisha kwa wakati ni kuifelisha dhamira njema ya Rais Dkt Hussen Mwinyi ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.
Mhe.Hemed amesema kukamilika kwa miradi ya maegesho ya magari iliyopo Kijangwani na Malindi Mjini Unguja na Nyumba za bei nafuu zilizopo viwanja vya Magereza kutawaondolea wananchi changamoto ya makaazi pamoja na msongamano wa kuegesha magari sehemu zisizo salama jambo linalopelekea kupotea kwa haiba ya mji Mji wa Zanzibar.
Sambamaba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza kuwa Serikali haitakuwa na muda wa nyongeza kwa Mkandarasi yoyote ambae atashindwa kukamilisha miradi aliyopewa kwa wakati na kuwaagiza washauri elekezi kutoa adhabu ya penalt kwa kampuni itakayokwenda kinyume na makubalino ya kimkataba.
Aidha Mhe.Hemed ametoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kuendelea kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Mwinyi za kuondoa changamoto mbali mbali zinazowakabili sambamaba na kuwaletea maendeleo wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Nae Naibu Waziri wa fedha na mipango Zanzibar Mhe. JUMA MAKUNGU JUMA amesema miradi inayojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) inaendana na dhamira ya viongozi ya kuweka mzingira bora kwa kila mwananchi hivyo Serikali kupitia Wizara ya fedha itahakikisha inasimamia vizuri ujenzi wa miradi hio kwa maslahi ya Taifa.
Mhe. Juma amesema majengo hayo yatawasaidia wafanya biashara kufanya biashara zao bila ya usumbufu wowotea na amewatoa hofu wanachama wa ZSSF kuwa fedha zao wanazochangia katika mfuko huo zipo salama na kila mwanachama atapatiwa haki yake kwa mujibu wa michango aliyochangia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hfadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Bwana Nassor Ameir Shaaban amesema ZSSF imekusudia kujenga vituo vitano(5) vya kisasa vya maegesho ya magari vitakavyotoa huduma ndani ya mji wa Zanzibar.
Amesema ZSSF imedhamiria kuwaondoshea wananchi wa Zanzibar changamoto ya huduma ya usafiri wa daladala ambapo imejipanga kutafuta kampuni ambayo italeta mabasi makubwa na ya kisasa yatakayotoa huduma ya usafiri ndani ya Zanziba